Umoja wa Mataifa wameonya kuwa mzozo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati
unakaribia kuwa janga, huku nusu ya idadi ya watu wakiachwa bila makaazi
tangu machafuko ya kimadhehebu yalipozuka
Mkuu wa masuala ya kisiasa wa Umoja wa Mataifa Jeffrey Feltmasn
ameliambia Baraza la Usalama kuwa karibu watu milioni 2.2 katika Jamhuri
ya Afrika ya Kati wanahitaji msaada wa dharura wa kiutu, ambayo ni
karibu nusu ya idadi jumla ya watu nchini humo. Takribani nusu ya watu
katika mji mkuu Bangui, ambao ni zaidi ya nusu milioni wametoroka
makwao, huku wengine 100,000 wakifurika katika kambi moja ya muda katika
uwanja wa ndege karibu na mji mkuu.
Rais wa sasa Michael Djotodia ambaye alichukua mahali pa Francois Bozize baada ya mapinduzi
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia watoto - UNICEF
lilionya mwishoni mwa mwezi Desemba, kuwa watoto wanaingizwa vitani, na
likathibitisha vifo vya watoto 16 tangu Desemba 5. Wawili kati ya watoto
hao walichinjwa.
Wakati huo huo, Mali na Senegal zimewahamisha mamia ya raia wao
wanaotoroka mapigano nchini humo. Katika mji mkuu wa Mali, Bamako,
waziri anayehusika na zoezi la kuwahamisha raia, Abdramane Sylla pamoja
na maafisa wengine wawili walikaribisha kundi la karibu watu 270
waliorudishwa nyumbani kwa kutumia ndege iliyokodishwa na serikali.
Waziri Sylla amesema ndege nyingine itaihamisha hii leo idadi nyingine
kama hiyo ya raia wa Mali. Zaidi ya Wamali 3,000 wanalikuwa wakiishi
katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Lakini kufikia sasa ni 500 pekee
waliosema wanataka kurudi nyumbani. Wengi wa waliohamishwa ni wanawake
na watoto, wengi wao waliozaliwa nchini humo na wazazi wa Mali waliokuwa
wakiishi nchini humo kwa muda mrefu.
Wanajeshi wakijaribu kuutuliza umati wa waandamanaji mjini Bnagui
Senegal imesema imewahamisha karibu raia 600 katika kipindi cha
chini ya wiki moja, kwa mujibu wa maafisa mjini Dakar. Shirika la
habari la Senegal, APS limeripoti kuwa serikali imewasafirisha raia wa
Guinea, Mali na Gambia ambao walikuwa wamekwama katika mzozo wa Afrika
ya Kati, lakini haikutoa idadi kamili.
Nigeria ilisema siku ya Jumapili kuwa inawaondoa raia wake 1,600 ambao
walitafuta hifadhi katika ubalozi wake mjini Bangui. Jamhuri ya Afrika
ya Kati yenye utajiri wa raslimali, imekumbwa na ongezeko la machafuko
tangu mapinduzi ya mwezi Machi, ya muungano wa waasi wa SELEKA uliokuwa
na waislamu wengi ulipomweka madarakani Michael Djotodia kama rais wa
kwanza wa nchi hiyo Muislamu.
Ijapokuwa Djotodia alilivunja kundi hilo la waasi, baadhi yao
waliendelea na vurugu, na kusababisha miezi kadhaa ya matukio ya mauaji,
ubakaji na wizi, hali iliyowalazimu Wakristo kuunda makundi ya
kujikinga. Majeshi ya Ufaransa na Umoja wa Afrika yamekuwa yakijaribu
kurejesha utulivu katika nchi hiyo tangu yalipotwikwa mzigo huo mwezi
uliopita na Umoja wa Mataifa. Zaidi ya watu 1,000 wameuawa katika
kipindi cha mwezi mmoja uliopita pekee, wakati wengine karibu nusu
milioni wakiwachwa bila makaazi, tangu mapinduzi.