Mrembo huyo
alikamatwa Desemba 19, mwaka jana katika Uwanja wa Ndege wa Macau
akitokea Bangkok, Thailand akiwa na kete 57 (kilo 1.1) za unga aina ya
heroin tumboni zikiwa na thamani ya shilingi milioni 300.
TAARIFA MBICHI
Taarifa mbichi kabisa zinadai
kwamba, Jack amepewa mwaka mmoja na nusu (siku 447) ajifunze lugha
inayozungumzwa na watu wa Macau (Kireno) ambayo ndiyo itakayotumika
mahakamani wakati kesi yake itakapoanza kuunguruma.
Dawa za kulevya alizokutwa nazo Jack Patrick.
Sheria ya kisiwa hicho inasema kuwa mshitakiwa yeyote atakayefikishwa
kortini, kesi yake haitasikilizwa mpaka majaji wakubali kwamba anajua
lugha hiyo na si kinyume na hapo.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, mwalimu maalum anayejua Lugha za Kiingereza na Kireno ndiye atakayemfundisha Jack mpaka atakapojua.
AKIJUA MAPEMA ITAMSAIDIA
Habari za ndani kutoka
vyanzo vya uhakika nchini humo zinasema kwamba, kama Jack angekuwa
anakijua Kireno angepandishwa kizimbani mara baada ya upelelezi
kukamilika, Machi mwaka huu.
KIFUNGO CHA CHINI MIAKA 16
Habari nyingine mpya
kutoka Macau zinasema kuwa, sheria za eneo hilo kuhusu makosa ya kukutwa
na madawa ya kulevya, mtuhumiwa akitiwa hatiani kifungo cha chini ni
miaka 16 kulingana na mwenendo wa kesi.
SERIKALI YA TANZANIA YASUBIRI ORODHA…
Juzi, Uwazi
liliwasiliana kwa simu ya mkononi na Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na
Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa na kumuuliza
kuhusu nini kinaendelea kati ya serikali na utawala wa Macau kufuatia
Mtanzania, Jack Patrick kunaswa na unga nchini humo.
Nzowa: “Aaah! Sisi tumetuma maswali yetu kule (Macau) kupitia Polisi
wa Kimataifa (Interpol), tumetaka kujua kama huyo binti (Jack) amewataja
vigogo waliomtuma ni majina gani wanayo.
“Ndiyo tunasubiri majibu
yao ili tujue nini kinaendelea kule. Kama aliwataja watu tutaanza
kuwafuatilia mara moja maana lazima kuna vigogo nyuma yake.”
KWA NINI MABOSI WA KUBEBA UNGA HUWA HAWATAJWI?
Kinachomshangaza Kamanda Nzowa ni usiri wa watu wanaodaiwa kukamatwa na unga kufunga vinywa vyao kuwataja vigogo waliowatuma.
Inadaiwa
moja ya kiapo kikubwa kabla mtu hajaanza kuwa ‘punda’ (kubebeshwa
madawa ya kulevya) ni kusema ‘piga, ua, galagaza’ katu hawezi kutaja
wahusika wenye mzigo.
“Unajua kwa sababu gani? Wale wanaobeba wanaambiwa mkikamatwa
msitutaje hata iweje ili tufanye mipango ya kuwatoa. Sasa mtu anaona
nikitaja sintatoka, ndiyo anaamua kuendelea kuishi na siri yake halafu
na wao wakubwa wao wanakuwa hawana habari nao,” alisema Nzowa.
KUMBE JACK ALIPEWA MAJI YA MOTO
Habari
zaidi zinasema kuwa, siku ya tukio la kukamatwa, Jack alikataa kwamba
hajabeba kete za unga tumboni, askari wa uwanjani wakampa maji ya moto
ili anywe.
“Kwa mtu aliye na kete tumboni, hawezi kukubali kunywa
maji ya moto kwani huyeyusha kete zilizomo ndani na kuweza kusababisha
kifo chake.
“Jack alikataa kunywa maji ya moto, hilo likachangia askari kuamini
ana kete tumboni, ndiyo maana walimpeleka chooni kuzitoa kitaalam,”
kilisema chanzo.
RAY C AWASHANGAZA WENGI
Kufuatia sakata la Jack,
hivi karibuni, staa wa muziki wa kizazi kipya Tanzania, Rehema Chalamila
‘Ray C’ aliingiza kwenye mtandao wake wa kijamii akitoa maoni kwamba
Jack apewe adhabu kali zaidi ya kifungo (pengine kunyongwa) hali
iliyowashangaza wengi waliotembelea mtandao huo.
Baadhi ya watu waliozungumza na Uwazi baada ya staa huyo kuingiza mawazo yake walimshutumu wakisema alitakiwa kutafakari upya.
“Yule dada (Ray C) hakutakiwa kumtakia mwenzake mabaya zaidi, kama
yeye aliathirika na madawa na amepona anatakiwa kuwa balozi kwa wengine
na si kuwahukumu wenzake,” alisema Joan Mushi, mkazi wa Sinza ‘E’ jijini
Dar.
WAZIRI MEMBE VIPI?
Juzi, Uwazi lilimtafuta Waziri wa Mambo ya Nchi
za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Kamillius Membe ili
azungumze lolote kuhusu sakata la Jack Patrick lakini hakupatikana
badala yake naibu wake, Mahadhi Maalim alisema taarifa za Jack
kukamatwa amezisikia kupitia vyombo vya habari na hana habari kiundani
ila bosi wake anaweza kuwa na maelezo zaidi.
WOLPER, AUNT EZEKIEL, WEMA, WANAWINDWA KUWA ‘MAPUNDA’
Wakati
Jack akiwa katika mazito hayo, habari ambazo zilifika kwenye dawati la
Uwazi dakika za mwisho zinasema mastaa wa filamu za Bongo, Jacqueline
Massawe Wolper, Aunt Ezekiel Grayson na Wema Isaac Sepetu wamekuwa
wakitolewa udenda na vigogo wa unga.
Vigogo hao wamekuwa wakihaha kutafuta namna ya kuwaingiza mastaa hao
kwenye ‘chaneli’ yao ili wawe mapunda wa kubeba kete za unga kupeleka
ughaibuni wakiamini kuwa, mastaa hawakamatwi hovyo uwanja wa ndege,
hususan wa Dar es Salaam.
chanzo glopal