Wakati Jeshi la Polisi likitoa
visingizio kwamba linashindwa kunasa watuhumiwa wanaosafirisha dawa za
kulevya wanaopitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA), kutokana na kukosekana kwa vitendea kazi, Mbunge wa Kinondoni
(CCM), Idd Azzan, amesema yupo tayari kupigwa risasi au kunyongwa
hadharani kama itathibitika anahusika na biashara hiyo.
Azzan alitoa kauli hiyo jana wakati
akihojiwa na kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Radio One kuhusu
kuwapo kwa madai ya barua iliyoandikwa na Mtanzania aliyefugwa Hong
Kong nchini China akimtaja kuhusika na biashara ya dawa hizo.
Alisema hahusiki kwa namna yoyote ile
na biashara ya dawa za kulevya au biashara yoyote haramu na kwamba
taarifa zilizoandikwa kwenye mitandao ya kijamii ni za upotoshaji na
zimetolewa kwa lengo la kumchafua.
“Nimejipeleka polisi kwa mara
nyingine tena na nimewaomba wafanye uchunguzi wa kina na kama
nitabainika nahusika na biashara hiyo niko tayari kupigwa risasi
hadharani, lakini pia sitendewi haki kwa wale ambao wanazusha jambo hili
wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema.
Azzan aliongeza kuwa hayupo juu ya
sheria hivyo ikithibitika kuna mtu anamtuma dawa za kulevya kupitia
bandari fulani pia atakuwa tayari kuwekwa hadharani na kunyongwa maana
atakuwa hafai kuendelea kuwapo Tanzania.
Alisema makundi yanayomwandama ni ya kisiasa kwa lengo la kutaka kumdhoofisha katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015.
Mahojiano kati ya Azzan na radio yalikuwa kama ifuatavyo;
RADIO: Mhe Idd Azzan wewe ni mbunge
wa Kinondoni inaelezwa kuwa wewe ni mmoja kati ya watu wanaojihusisha na
dawa za kulevya na mmekuwa mkipokea mizigo kupitia maboti makubwa
yanayotoka Pakistan yanayopitia Bagamoyo, Tanga, Mtwara na Dar es
Salaam, hebu tujuze na wajuze Watanzania hili lina ukweli gani.
AZZAN: Hata mimi nimesikia hilo na
bahati nzuri nimesoma kwenye mitandao kadhaa imeandika hivyo na kuna
barua inayodaiwa kuandikwa na mfungwa mmoja ambaye amedai mimi ndiye
nahusika kumtuma yeye.
Napenda kuwajulisha Watanzania
sihusiki kwa namna yoyote ile na biashara ya dawa za kulevya na siyo
dawa za kulevya tu lakini pia biashara yoyote haramu sijawahi kufanya
katika maisha yangu.
Niseme tu kuwa hizo ni taarifa ambazo
zimetolewa kwenye mitandao ili kuaminisha watu hivyo, lakini kimsingi
sihusiki na sijihusishi na biashara ya namna hiyo.
Baada ya kuziona habari hizi kwenye
mitandao nilichokifanya na sababu ilishawahi kujitokeza tena na viongozi
wangu wa CCM walishawahi kuyasema hayo kwenye mkutano wa vijana
nikawaambia polisi wachunguze ili kupata ukweli wa hilo jambo.
Kama itabainika nahusika basi
nichukuliwe hatua za kisheria mimi siyo Mungu wala sipo juu ya sheria,
nimefanya hivyo kwa maana ya kuongea na Jeshi la Polisi nimejipeleka
nimetoa maelezo na nimewataka polisi kwa sababu ni kazi yao wafanye
uchunguzi wa kina, pili kama nahusika na tuhuma hizo hatua za kisheria
zifuatwe dhidi yangu na kama siyo kweli hao wanaoeneza uzushi huo pia
wachukuliwe hatua.
RADIO: Unadhani kwa nini Mtanzania aliyeshikiliwa Hong Kong amekutaja wewe kuhusika na biashara hiyo?
AZZAN: Kwanza mimi siamini kwamba
kuna Mtanzania anayeshikiliwa Hong Kong ambaye amenitaja mimi, sababu
hiyo biashara kwanza sijawahi kuifanya, mimi niliiona hiyo barua haina
jina la huyo Mtanzania mnayemsema, wala hakuna namba ya mfugwa sasa
mfungwa anatakiwa kuwa na namba, asitaje jina ataje basi walau namba
yake pia hakuna jina la gereza, kwa hiyo mimi siamini Mtanzania ambaye
amefugwa kwa tuhuma za dawa za kulevya anitaje mimi kuwa nimemtuma.
Hakuna hicho kitu na hakuna Mtanzania ambaye niliwahi kumtuma hicho kitu
kimetengenezwa kwa nia ya kunichafua.
RADIO: Mheshimiwa unatafsiri vipi tukio hili?
AZZAN: Mimi ninachotafsiri tayari
mapambano ya 2015 ndiyo yanaanza na watu wanatafuta jinsi ya kunichafua
sababu hata tukienda kwenye kura nitawashinda, lakini si kutafuta mbinu
chafu za kunichafua.
Yapo maneno ambayo nayazungumza
bungeni hayawafurahishi wengine, lakini kwa Watanzania wengi yana
manufaa, kwa hiyo kwa wale ambao hayawafurahishi wanaweza wakawa
wamechangia katika kunichafua.
RADIO: Lakini Mheshimiwa Idd Azzan
mara nyingi tu umekuwa ukitajwa na watu mbalimbali kwamba unajihusisha
na uuzaji wa dawa za kulevya ama wewe ni mmoja kati ya watu wanaowaagiza
watu mbalimbali kusafirisha mizigo hiyo ya dawa za kulevya hilo kwa
upande wako unalizungumza vipi.
AZZAN: Nasema binafsi nimejipeleka
polisi na nilishajipeleka mara ya kwanza baada ya kutokea tuhuma kama
hizi, nikawaambia polisi wafanye uchunguzi kama nahusika nichukuliwe
hatua za kisheria, nimekwenda tena kuwaambia polisi na nasisitiza polisi
wafanye uchunguzi wa kina kama nahusika hatua za kisheria zichukuliwe
dhidi yangu.
Kama nitabainika nahusika na biashara
hiyo niko tayari kupigwa risasi hadharani, lakini pia sitendewi haki
kwa wale ambao wanazusha jambo hili wachukuliwe hatua za kisheria.
RADIO: Lakini Mheshimiwa kwa upande
mwingine tayari taarifa zimeshatolewa kama hivyo kwenye mitandao
mbalimbali ya kijamii, sasa endapo itabainika kweli umehusika ama
hujahusika ni kitu gani ambacho utakifanya.
AZZAN: Naomba niweke wazi kama
itathibitika ninamtuma mtu madawa ya kulevya kupitia bandari gani mimi
nipo tayari kuhukumiwa sababu sipo juu ya sheria na pia nipo tayari
niwekwe hadharani waninyonge sifai kuendelea kuwapo Tanzania kama
nahusika na hilo, na kama sihusiki serikali initendee haki kwa watu
wanaosambaza uvumi huu nao wachukuliwe hatua siyo wakae tu na kumrushia
mtu vitu vya uongo.
Awali Kamanda wa Polisi Viwanja vya
Ndege, Deusdedit Kato akihojiwa katika kipindi hicho juu kwanini JNIA
umeonekana kuwa kitovu cha kupitishia dawa za kulevya, alisema sababu
kubwa ni kwamba kuna tofauti kati ya nchi na nchi katika masuala ya
teknolojia katika kubaini dawa za kulevya.
Kamanda Kato alisema nchi nyingine
wana vifaa vya kisasa zaidi na kwamba wakati sasa umefika kwa serikali
kuwekeza katika kupata vitendea kazi zaidi ili kufanikisha mapambano ya
dawa za kulevya.
Aliongeza kuwa wamekuwa
wakishirikiana na viwanja vingine vya nchi mbalimbali kwa kubadilishana
taarifa lengo likiwa ni mapambano ya biashara hiyo.
“Kimsingi wanaokamatwa wanakuwa ni
wabebaji tu na siyo matajiri wa dawa za kulevya, bahati mbaya wabebaji
wamekuwa wagumu sana kutoa ushirikiano kwa polisi, nasisitiza vitendea
kazi vinachangia kuponya mtu asikamatwe nchini na kwenda kukamatwa nje,”
alisema.
Kamanda Kato alisema katika kipindi
cha miezi sita hadi nane watu 14 wamekamatwa wakituhumiwa kusafirisha
dawa za kulevya nchini.
•Julai 5, mwaka huu wasichana wawili,
Agnes Jerald (25) na Melisa Edward (24), walipita JNIA na shehena ya
dawa za kulevya kilo 150 na walikamatwa Afrika Kusini na kushtakiwa
nchini humo kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya.
Hawa walikamatwa Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Oliver Tambo wakiwa na shehena ya dawa hizo aina ya Crystal
Methamphetamine zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 6.8.
•Ijumaa wiki iliyopita yaani Julai
26, mwaka huu, Watanzania wengine wawili, walikamatwa Hong Kong wakiwa
na dawa za kulevya aina ya cocaine na heroine zenye thamani ya Sh.
bilioni 7.6 akiwamo mmoja aliyekamatwa akitokea Dar es Salaam kupitia
Dubai hadi Hong Kong.
Taarifa kutoka Hong Kong za Ijumaa
wiki iliyopita zinaeleza kwamba, maofisa ushuru wa Uwanja wa Ndege wa
Hong Kong (HKIA), walimkamata kijana mmoja mwenye umri wa miaka 26
akitokea Tanzania na alikuwa na dawa za kulevya aina ya heroine kilo 1.6
zenye thamani ya Sh. bilioni 1.5, kwenye mzigo wake wa mkononi.
•Siku hiyo hiyo jioni, maofisa hao
walimkamata Mtanzania mwingine mwenye miaka 45 ambaye alipelekwa
hospitali na kutolewa gramu 240 za dawa za kulevya aina ya heroine.
Taarifa zaidi zilieleza kuwa Mtanzania mwingine mwenye miaka 28
alikamatwa akiwa na kilo 2.03 za cocaine.
Source: Nipashe.
0 Maoni Kuhusu Habari Hii