Sisi tu Masikini wa Maadili na Uchumi pia, tatizo letu nini?


Katika maandalizi ya kuuanza mwaka mpya 20I4, tulikuwa tukiomba na kutakiana heri ili kila mmoja wetu aweze kuumaliza vizuri mwaka 20I3 kwa amani, bila dhahima yeyote. Pamoja na juhudi zetu katika kutakiana heri ya mwaka mpya 20I4 na kuhimiza uwajibikaji kikamilifu juu ya usalama wetu wakati tunaposafiri kwenda kusherehekea sherehe hizo za mwisho wa mwaka kwa kuruhusu ajari nyingi kutokea barabarani na hivyo kupelekea ndugu na jamaa zetu wengi kupoteza maisha. Ni ukweli usiopingika kuwa sisi sote tumekuwa sehemu ya matukio haya ya kusikitisha kwa namna moja ama nyingine kutowajika kila mtu kwa nafasi yake..
Sisi kama Watanzania, ili tutambulike na kuheshimika kama taifa kubwa na lenye nguvu tunahitaji mambo mawili muhimu ambayo ni kuwa na jamii safi kimaadili, pamoja na uchumi imara. Yote haya hujengwa na kusitawishwa katika misingi ya utawala bora na uliotukuka.
Utawala bora ni utawala wa sheria unaolinda jamii dhidi ya matendo ya kidhalimu ya watawala dhidi ya watawaliwa. Mahakamani kwa mfano, Hakimu anapaswa kuwa muadilifu na mtiifu kwa haki kuliko chochote, iwe serikali au mtu yeyote. Kwa maana nyingine ni kwamba kesi zinazofanana ni lazima ziwe na matokeo yanayofanana. Huo ndio utawala bora na ambao ndio chemichemi ya jamii inayoheshimu sheria na muumini wa haki na usawa.
Msingi wa jamii imara yeyote ile duniani ni haki. Na haki hii, hutekelezwa na kusimamiwa na serikali ya jamii husika juu ya wanajamii. Serikali dhaifu katika usimamizi wa haki huzaa rushwa baina ya wasimamizi wa sheria na wasimamiwa. Huzaa ajari za barabarani. Huzaa uonevu. Na zaidi ya yote huzaa jamii haramu. Swali, ni namna gani jamii haramu hutokea?
Nikiwa chuo kikuu nasoma mwaka wa pili nilibahatika siku moja, kukaa na wasichana wanne katika meza moja ya chakula. Tukiwa tunaendelea kula, nilisikiliza maongezi ya wasichana hao yaliyohusu mahusiano yao ya kimapenzi. Maongezi yao waliyajengeka katika mtazamo wa jinsi gani ilivyo batili kwao kuolewa na Mwalimu. Katika kujenga hoja walidai mshahara wa mwalimu ni mdogo, hivyo hautoshi katika kuendesha maisha.
Nikiwa kama mwanafunzi niliyekuwa nasoma shahada ya ualimu, niligundua kuwa kama ningelikuwa natafuta mke wa kuoa, basi sikuwa na sifa ya kumuoa yeyote yule katika lile kundi kwa vile nilikuwa mwalimu mtarajiwa. Walidai kuwa mwalimu hutoka nyumbani asubuhi na kurudi jioni mikono mitupu iliyojaa vumbi la chaki. Kwao waliona kuwa ni heri kuolewa na jambazi kuliko kuolewa na mwalimu. Nilihamaki ghafla nikaondoka zangu nikihofia wangeniharibia siku.
Mtazamo huu si tu kwa wasichana hawa bali kwa jamii nzima. Na mtazamo huo haramu ulianzishwa na kusitawishwa katika jamii hii hii. Nao ukazaa matunda haramu. Lakini yana msingi wake, nayo ni kushamiri kwa rushwa katika jamii na kuwa kama sehemu ya tamaduni zetu. Hii ndiyo jamii tuliyomo, kwao ni heri nchi iongozwe na tajiri anayenuka rushwa kuliko kuongozwa na mtu ambaye ni maskini, mwadilifu na mtendaji mzuri.
Sisi kama taifa, ili tusafishe taswira ya taifa letu mbele ya mataifa mengine na kunusuru uzao wetu wa kesho, yatupasa tujitazame na kujitathimini upya tumetoka wapi, tuko wapi na tunaelekea wapi?. Afya ya maadili inapaswa kujengwa na kulindwa kuanzia kwa viongozi wetu wa juu kabisa wa taasisi zote,zikiwemo za kisiasa, kiuchumi na za kijamii. Tuilinde na kuiishi katika misingi ya haki kuanzia katika jamii, familia na hatimae mtu mmoja mmoja. Huko ndiko kujenga jamii bora na yenye maadili. Swali, ni namna gani tunaweza kujenga uchumi wetu? Na kwa nini serikali imeshindwa kumea maisha bora(prosperity life) kwa kila mtanzania kama ilivyoahidi?
Katika kitabu chao cha “The origins of power, prosperity and Poverty. Daron Acemoglu na James Robinson” wanaelezea kwa nini baadhi ya mataifa kwa mfano Botswana, ni moja ya mataifa duniani ambayo uchumi wake unakuwa haraka zaidi kuliko mataifa mengine kama Congo, Zimbabwe na Sierra leon, ambayo yamebaki kwenye umasikini wa kutupwa na vita.
Kwa kutumia mfano wa jiji la Nogoles, Daron na James wanadai kuwa katikati ya jiji la Nagoles kuna ukuta unaoligawa jiji hili sehemu mbili, nazo ni Nagoles ya kaskazini na Nagoles ya kusini. Wanadai ukisimama juu ya ukuta ukatazama kaskazini utaona mji wa Nagoles ya Arizona. Hii iko katika jimbo la Santa cruz, nchini Marekani. Kipato cha wakazi wa Arizona ni takribani $30,000 kwa mwaka. Watoto wote wenye umri wa kusoma wako shule. Watu wazima walio wengi wamehitimu Vyuo vikuu. Wana uhakika na matibabu ya bure kutokana na sera ya Rais Barack Obama(Obama’s health care). Karibu jamii yote ina afya na muda mrefu wa kuishi (takribani miaka 65). Wanao uhakika wa huduma nyingine kama Umeme, Mawasiliano, Usafiri, Sheria na mamraka.
Huenda kwenye shughuli zao za kila siku bila hofu ya maisha au usalama wao, na hawaogopi wezi, kutaifishwa wala masharti ya kuwekeza katika biashara zao. Wanaishi kwa haki na usawa na serikali ndiyo wakala wa haki na suluhisho la matatizo yao. Na zaidi ya yote, wanaheshimu demokrasia.
Lakini katika upande mwingine kusini mwa ukuta, Nagoles Sonara, hatua chache kutoka kwenye ukuta ni tofauti kabisa. Kipato cha wakazi wa Sonara kwa mwaka ni robo ya kipato cha wakazi wa Arizona. Watu wazima wengi hawajahitimu elimu ya chuo kikuu na watoto wengi hawaendi shule. Hofu imetanda kwa kina mama mjamzito kutokana na vifo vingi kwa akina mama wajawazito vinavyosababishwa na huduma duni katika taasisi za afya. Barabara ni mbovu. Sheria hazimpi raia haki ya kuwekeza. Wanasiasa wa Sonara ni Waumini wa rushwa na wabadhirifu kupindukia.
Na mwisho kabisa, Daron na James wanahitimisha kwa kudai kwamba ‘‘ It’s man-made political and economic institutions that underlie economic success (or lack of it)’’. Kwa tafsiri isiyo rasmi ni kwamba “ ni taasisi za kisiasa na kiuchumi pekee ndiyo zenye uwezo wa kukuza au kudumaza uchumi katika nchi husika.
Hivyo kwa kuzingatia ushawishi wa akina Daron na James sanjari na marejereo rukuki niliyonayo kutokana na historia ya nchi yangu na nchi nyingine za kiafrika, napenda nisema kuwa umasikini tulionao umetokana na utashi wa viongozi wetu. Viongozi wetu hawana nia njema ya kustawisha taasisi zetu za kiuchumi na za kisiasa.
Taasisi zetu, mfano taasisi za kifedha kama Bank kuu(BoT) haitekelezi wajibu wake katika misingi ya kizalendo bali imeachia mianya ya kinyonyaji kutawala katika mfumo wa fedha. Taasisi hii imekuwa dhaifu mno katika kupambana na udharimu(criminality) unaokuwa kila kuchapo ndani ya taasisi hii mhimu katika michakato ya kimaendeleo ya nchi.
Kutokana na kelele za mataifa mengi tajiri duniani juu ya nchi masikini kuhifadhi fedha nje ya nchi, haihitaji hata upeo upitao upeo wa kawaida kubaini kuwa kuna watanzania wengi wametunza fedha zao nje ya nchi, ziwe zilipatikana kwa njia halali au haramu. Kutunza fedha nje ya nchi ni matokeo hasi ya taasisi za kifedha (financial institution) kushindwa kuwahakikishia watu wake usalama wa mitaji yao kipindi uchumi wa nchi unapotetereka. Hivyo watu huamua kuwa ni heri wapeleke fedha zao pahala ambapo patawahakikishia uhai wa mitaji yao bila kujali madhara yanayoipata nchi yao kutokana na maamzi yao. Athari tunazozipata hapa ni kudhoofika kwa mifumo yetu ya kifedha kwani msingi wa fedha ni fedha.
Taasisi hii pia imeshindwa kudhibiti mfumko wa riba za juu zinazotozwa na mabenki madogo madogo kwa wateja wao. Mabenki haya hayawakopeshi wajasiliamali na wafanya biashara wadogo wadogo kwa misingi ya kizalendo ili kunusuru na kukuza mitaji yao bali kwa misingi ya kinyonyaji. Haziwawezeshi wakulima kupata pembejeo wala kuwatafutia na kulinda soko la bidhaa zinazotokana na viwanda vinavyotengeneza mali ghafi zao.
Hata hivyo uimara wa taasisi za kiuchumi hauwezi kuonekana bila kuwepo kwa taasisi imara za kisiasa(political institutions). Hizi ndizo zinazopanga sera na mikakati ya kimaendeleo na kuhakikisha zinasimamiwa kwa misingi ya ilani ya chama kilichopo madarakani.
Bahati mbaya sana nchini Tanzania na Barani Afrika kwa ujumla, nguvu za kisiasa hutafsiriwa kama dhana ya mafanikio na maisha bora kwa mwanasiasa husika. Siyo tu kwa anayeshika madaraka hayo bali pia kwa familia yake, uzao wake na ikiwezekana hata eneo alilozaliwa. Mtazamo huu umejengwa katika msingi wa ubadhirifu, unyonyaji, ufisadi na kutowajibika.
Katika ripoti yake ya transnational crime in the developing world, Jeremy Haken 2024 anadai nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania hupoteza dolar trillion moja kwa mwaka kupitia njia haramu za mifumo ya kifedha(illicit finacial flow, IFF) ambazo hutokea katika nyanja tatu nazo ni pamoja na rushwa kupitia kwa wanasiasa na watumishi wa umma(political corruption), nayo huchukua 3%. Pili uharamia wa kimataifa(international crime), yaani wizi utokanao na biashara haramu kama madawa ya kulevya, utoroshaji wa fedha nje ya nchi(money laundering), biashara za watu, nyara za serikali n.k (nao ni takribani 35%). Wizi wa tatu ni ule unaotokana na ukusanyaji duni wa mapato(commercial transactional) nao ni ukwepaji wa kulipa mapato stahiki, ambao ndiyo umeenea kila kona ya nchi yetu. Huu huchua 62% iliyobaki. Hii huhusisha ukadiriaji wa juu kwa bidhaa zinazoingizwa nchini na ukadiriaji wa chini kwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi. Bila ya shaka Tanzania ni moja ya Wahanga na wathirika wa mfumo huu dharimu na hatari kwa ustawi wa uchumi na jamii kwa ujumla.
Ili kuzishinda changamoto hizi na kuhakikisha uchumi wetu unakua na kumea maisha bora kwa kila mtanzania, hatuhitaji kiongozi mwenye sifa za urais pekee, bali twapaswa kutafuta na kupata kiongozi mwenye sifa zaidi ya uongozi. Kiongozi atakayetutoa tulipopotekea na kutupeleka tunapotaka kwenda. Kiongozi atakayehakikisha taasisi za kiuchumi na kisiasa zinafanya kazi kwa pamoja katika kuhakikisha maendeleo ya nchi yanafikiwa.


Vielezo:

Swahili Zone

Tovuti huru habarishi (blogu) inayoendeshwa kiueledi yenye lengo mahususi la kuifikishia jamii habari, makala na matukio wakati muafaka inapowezekana kufanya hivyo!

0 Maoni Kuhusu Habari Hii

Andika Maoni Yako