Kikosi Kazi cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Uwanja wa Ndege wa Dar es
Salam (JNIA) jana kilimkamata mwanamke mmoja, Salama Omari Muzara akiwa
amemeza kete za dawa za kulevya aina ya Heroin ambazo idadi yake kamili
haijajulikana.
Kamishna wa Polisi Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey
Nzowa alisema, msichana huyo alikamatwa jana saa saba mchana akiwa
njiani kuelekea Macao, China na Shirika la Ndege la Ethiopia.
“Alikuwa anasafiri kwenda Macao, China kwa ndege ya Ethiopian Airlines
ambayo ilikuwa iondoke saa 10 jioni ndipo kikosi kazi cha polisi uwanja
wa ndege kikamshuku kuwa amebeba kitu kisicho cha kawaida” alisema
Nzowa.
Nzowa alisema, mwanamke huyo alikuwa na hati ya kusafiria namba AB548242
ambayo ilitolewa Oktoba mwaka jana na haikufahamika idadi kamili ya
pipi alizomeza kwani mpaka sasa bado anazitoa. Nzowa alisema mpaka sasa
mwanamke huyo tayari ameshatoa pipi kadhaa tangu alipokamatwa jana
mchana ambapo kuanzia asubuhi leo hadi saa saba mchana huu ameshatoa
pipi 27.
Kamishna Nzowa alisema hiyo ni sehemu tu ya mapambano ya dawa za kulevya
nchini ambayo imesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa wasafirishaji na
watumiaji wa dawa hizo.
Hivi karibuni, Mwanamitindo wa Tanzania, Jackline Cliff alikamatwa na
kete 66 za dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya dola za
Marekani 137,720 huko Macao, China.
Mwanamitindo huyo , aliyekuwa akisafiri kutoka Thailand akielekea Macao
aliwaambia polisi kuwa alikuwa anaelekea Guangzhou ambao ni mji wa jimbo
la Guangdong huko China.
Kamanda Nzowa alisema kikosi chake kinaendelea kuwasiliana na Polisi wa
Macao ili kujua iwapo ataweza kurejeshwa nchini ingawa alikiri suala
hilo limekuwa gumu kwani China hawana utaratibu wa kubadilishana
wafungwa.
0 Maoni Kuhusu Habari Hii