Benki yafungua mlango wa biashara Tz-China


Benki ya Exim ya Tanzania imefungua huduma mpya ya Dirisha la Biashara la Tanzania-China, ili kukuza biashara baina ya nchi hizo.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim, Anthony Grant jana ilisema huduma hiyo mpya itawawezesha wateja kupata njia nzuri ya kufanya malipo ya bidhaa zinazoingia na kutoka kwa kutumia fedha ya China.
Grant alisema benki yake tayari imeingia ubia na Benki ya HSBC iliyopo mjini Hongkong na kuongeza kuwa, huduma hiyo mpya itatoa viwango vya riba vya ushindani kwa wafanyabiashara wa nchi hizo.
“Uanzishaji dirisha la biashara la Tanzania-China ni moja kati ya mikakati yetu ya kuendelea kupanua mahitaji ya benki yanayozidi kuongezeka baina ya wafanyabiashata wa nchi hizi,” alisema Grant na kuongeza:
“Kupitia huduma hii mpya, wafanyabiashara wa Tanzania na China watapata nafuu ya kutuma na kupokea fedha kwa urahisi.”
Pia, Grant alisema benki yake imeamua kufungua huduma hiyo mpya kutokana na kukua kwa biashara kati ya Tanzania na China kwa miaka ya karibuni.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), bidhaa zinazosafirisha kwenda China zimeongezeka kutoka dola 101 bilioni mwaka 2005 mpaka dola 908 bilioni kwa mwaka 2010.

Chanzo: Mwananchi Tovuti
Vielezo: , , ,

Swahili Zone

Tovuti huru habarishi (blogu) inayoendeshwa kiueledi yenye lengo mahususi la kuifikishia jamii habari, makala na matukio wakati muafaka inapowezekana kufanya hivyo!

0 Maoni Kuhusu Habari Hii

Andika Maoni Yako