Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete, ameondoka nchini kwenda Marekani kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.
Taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari jana,
ilisema kuwa Rais Kikwete aliondoka juzi Jumatano na kwamba kulingana na
ratiba ya uchunguzi wa afya yake anatarajiwa kurejea nchini Alhamisi ya
wiki ijayo.
Hata hivyo, taarifa hiyo iliyotolewa na Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais, haikueleza bayana tatizo linalomsumbua Kikwete
mbali ya kusisitiza kuwa amekwenda huko kwa ajili ya uchunguzi wa
kitabibu.
Taaarifa za hali ya afya ya Rais Kikwete kwa mara
ya kwanza ilitolewa mwaka 2009, ikiwa ni siku chache tu baada ya
kushindwa kukamilisha hotuba aliyokuwa akiitoa kwenye sherehe za miaka
100 ya Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) kwenye Uwanja wa
CCM Kirumba, Mwanza.
Rais Kikwete alilazimika kukatiza hotuba yake na
kwenda kwenye chumba cha mapumziko kwa muda wa dakika 10 kutokana na
kile kilichoelezwa na daktari wake kuishiwa nguvu.
Wakati huohuo, Mke wa Rais Mama Salma Kikwete
amewasili nchini jana akitokea Dubai, Falme za Kiarabu ambako alipata
Tuzo ya Dunia ya Hamasa ya Uongozi (Global Leadership Inspiration
Award), ambayo msingi wake ni kutambua uongozi madhubuti na hamasa
katika kutetea hadhi ya wanawake duniani.
Akizungumza tuzo hiyo alisema: “Tuzo niliyopata ni
heshima kubwa kwa wanawake wa Tanzania...hakuna maendeleo ya kweli na
endelevu bila wanawake, hivyo lazima jitihada zifanyike kushirikisha
wanawake katika sekta mbalimbali za maendeleo.” Mama Kikwete aliwataka
wanawake nchini kujitokeza kuzungumzia unyanyasaji wa kijinsia
wanaofanyiwa na wanaume.
chanzo mwananchi
0 Maoni Kuhusu Habari Hii