Moshi.Raia
watatu wa kigeni waliokamatwa hivi karibuni kwa nyakati tofauti katika
Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA), wakituhumiwa kusafirisha dawa za
kulevya wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi na kusomewa
mashtaka matatu tofauti
.
.
Watuhumiwa hao waliopandishwa kwa nyakati tofauti
katika mahakama hiyo, ni pamoja na Josian Crepy (25) raia wa Togo na
Julius Nyaoro, anayesadikiwa kuwa raia wa Kenya anayeishi Chanika
Tangini Dar es salaam na Grace Gratu (24) raia wa Liberia walikamatwa
mapema mwezi huu katika Uwanja wa ndege wa KIA .
Mtuhumiwa wa kwanza kupandishwa mahakamani hapo
alikuwa ni Grace Teta Gratu (24),ambaye alisomewa shtaka la kukamatwa
akiwa na kilo 10.5 za dawa za kulevya aina ya Cocaine.
Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Moshi, Simon Kobelo, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Janet Sekule
aliieleza mahakama kuwa, mtuhumiwa huyo anashtakiwa kwa kosa la
kusafirisha dawa hizo za kulevya nje ya nchi kinyume cha sheria.
Akisikiliza maelezo ya shtaka hilo, hakimu Kobelo
alisema kwa mujibu wa sheria ya dawa za kulevya kifungu namba 16 sura ya
95 ya mwaka 2002 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012 mahakama hiyo
haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.
Kwa mujibu wa sheria ya dawa za kulevya
iliyofanyiwa marekebisho kifungu cha 1 (a) makosa ya kusafirisha dawa
hizo yanasikilizwa na Mahakama Kuu na adhabu yake ukipatikana na hatia
ni kifungo cha maisha na kwamba kesi hizo hazina dhamana.
Shauri la pili lilikuwa ni la kula njama na
kusafirisha dawa za kulevya, watuhumiwa walikuwa ni Josian Dede Crepy
(25) wa Togo na mwenzie Julius Michael Nyaoro mkazi wa Chanika Tangini
Dar es salaam.
Akitoa uamuzi wa mahakama baada ya kusikiliza
maelezo ya mashtaka yote mawili, Hakimu Mkazi, Timotheus Swai alisema
kesi hiyo inasikilizwa na Mahakama kuu na kesi hiyo imeahirishwa hadi
Disemba 24, mwaka huu.
0 Maoni Kuhusu Habari Hii