Mfalme wa Jamii wa Wazulu nchini Afrika Kusini, Goodwill Zwelithini, anatarajiwa kutoa wito kwa raia wa nchi hiyo kujiepusha na ghasia, kufuatia kuongezeka kwa mashambulio ya kibaguzi nchini humo
.
Mfalme huyo ameshutumiwa kwa kuchochea mashambulio hayo ambayo yamesababisha vifo vya watu saba.
Zwelithini, alinukuliwa akisema kuwa raia wote wa kigeni wanapaswa kurejea katika mataifa yao.
Zaidi ya watu mia tatu wamekamatwa kuhusiana ghasia hizo.
Maelfu ya watu wanatarajiwa kufurika uwanja mmoja ulioko mji wa Mashariki wa Durban kusikiliza hotuba hiyo ya Mfalme Zwelithini.
Amekariri kuwa matamshi yake hayakufahamika.
Miongoni mwa washukiwa waliokamatwa hivi karibuni na wanaume watatu ambao wanatuhumiwa kuhusika na mauaji ya rais mmoja wa Mozambique katika eneo la Alexandra viungani mwa mji mkuu wa Johannesburg.
Picha kadhaa zimeonyesha Emmanuel Sithole akindungwa kisu huku umati mkubwa ukitizama.
Rais wa nchi hiyo Jacob Zuma, amesema mashambulio hayo yanakwenda kinyume na maadili yote wanayoamini.
Makundi kadhaa yaliyojihami yameshambulia na kupora maduka kadhaa yanayomilikiwa na wahamiaji kutoka mataifa mengine ya Afrika.
Huku idadi ya watu wasio na kazi nchini humo, ikikadiriwa kuwa zaidi ya asilimia Ishirini na nne, raia wengi wa taifa hilo wamewashutumu raia wa kigeni kwa kuchukua nafasi zao za kazi.
Maelfu ya raia hao wa kigeni, wamekimbia makwao na sasa wanaishi katika kambi za muda, ili hali mataifa jirani wameanza shughuli ya kuwahamisha raia wao.
Siku ya Jumapili, serikali ya Zimbabwe imetuma mabasi kadhaa mjini Durban kwenda kuwachukua raia wake wapatao mia nne.
Takwimu rasmi za serikali zinakadiria kuwa kuna raia milioni mbili wa kigeni wanaoishi nchini Afrika Kusini, lakini wengi wanahoji kuwa idadi hiyo huenda ni kubwa zaidi.
0 Maoni Kuhusu Habari Hii